MAANA YA WOKOVU






WOKOVU NI NINI?


Kuokoka si lugha mpya masikioni kwako msomaji! Mara nyingi umesikia kwa watu mbalimbli na katika maeneo tofautitofauti kuwa mtu fulani “amenusurika na janga la moto” au “ameokolewa kwenye moto” au “jeshi la nchi fulani limekomboamateka wake” au “ mtu amepona kwenye ajali mbaya”.

Yote haya yanaelezea hali ya kunusurika au kuokoka kutoka kwenye hali hatarishi au kwenye mateso makali. Hii ndio hasa maana ya kuokoka


Nini maana ya wokovu?


Kuokoka ni kunusurika, kusalimika, kukombolewa, kufunguliwa au kupona kutoka katika janga au hatari fulani.

Ili kuelewa hasa maana ya wokovu kibiblia, yakupasa kujua yafuatayo:




1. Mungu alituumba wanadamu kwa sura na mfano wake…!


Ni jambo la kushangaza lakini ndio uhalisia wenyewe. Mungu alimuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake.

Katika biblia tunasoma hivi… “Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba” [Mwanzo 1: 26,27]

Kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu maana yake ni kwamba roho ya mwanadamu iliumbwa iwe na matendo mema kama vile Mungu atendavyo. Mungu alikusudia mwanadamu awe na upendo, huruma, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi, n.k. Hivyo sura na mfano wa Mungu haimaanishi sura au umbo la kimwili bali ni roho. Adam na Hawa waliumbwa wakiwa na sura na mfano wa Mungu.


2. Lakini…

Mwanadamu alimtenda Mungu dhambi…!


Mungu alimweka Adam na Hawa kwenye bustani nzuri ya Edeni ili waitunze na kuishi humo. Mungu alimpa Adamu agizo la kula matunda ya miti yote bustanini isipokuwa matunda ya mti wa ujuzi wa  mema na mabaya.

Tunasoma hivi kwenye biblia… “Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika” [Mwanzo 2:16:17]

Lakini Adamu na Hawa walishindwa kutii sauti ya Mungu na kumwasi. Shetani aliyemjia Hawa kwa mfumo wa nyoka, ndiye aliye mdanganya. Soma Mwanzo 3:1 – 19
 

3. Hata ikawa ...

Wanadamu wote wametenda dhambi…


Dhambi aliyoitenda Adamu na Hawa imesababisha kuwepo kwa wanadamu ambao hawamchi Mungu. Kumeibuka kizazi ambacho kipo mbali sana na Mungu. Kimejaa  dhambi na uovu wa kila namna. Hata kudiriki kuua wanadamu kama vile mtu anavyo chinja kuku kwa ajili ya kula. Lakini biblia inasema kuwa dhambi ya Adamu ana Hawa ndiyo iliyo sababisha hayo yote; Hata wanadamu kuzaliwa kwenye hali ya dhambi.

“… kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.” [Warumi 3: 23]

Dhambi ni mbaya sana! Hututenga na uso wa Mungu. Hutufanya tuishi chini ya utumwa wa shetani na malaika zake. Dhambi huharibu maisha ya mtu hata kumfanya azeeke kabla ya wakati wake.


4. Bado...Mungu ametupenda sana kiasi cha kutuletea wokovu

Mungu bado ametupenda kiasi cha kutafuta namna ya kumwokoa mwanadamu kutoka kwenye utumwa wa shetani na dhambi.

Biblia inasema hivi … “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3: 16)

Hii ndio suluhisho au wokovu kwa mwanadamu. Yesu alikuja duniani akazaliwa kama mwanadamu kwa uwezo wa Roho mtakatifu, akahubiri na kufundisha habari za ufalme wa Mungu na hatimaye kufa msalabani kama dhabihu kwa ajili ya makosa, dhambi na uovu wote wa mwanadamu.

Biblia inasema hivi...

“....Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” [Mathayo 1:21]

 “Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” [Waefeso 2:4 – 6]

“... Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.” [Wakolosai 1:13,14]


Hii ndio maana halisi ya wokovu


Wokovu ni maisha mapya ambayo mtu anayapokea kwa imani baada ya kumwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Ni maisha ambayo Mungu anasamehe na kufuta dhambi zako zote ulizozitenda na wala hazikumbuki tena maana umemwamini Yesu Kristo aliyesulubiwa, akamwaga damu yake na kufa msalabani kwa ajili ya dhambi za wanadamu wote.

 Ndipo Biblia husema.....

“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; yakale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya.”[2Wakorintho 5: 17]

“Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.” [Warumi 5: 8,9]

“Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyo tupenda Mungu , Baba yetu.” [Wagalatia 1: 3,4]


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

IJUE BIBLIA - Sehemu ya I

HIVI NDIVYO MTU ANAVYOOKOKA