HIVI NDIVYO MTU ANAVYOOKOKA



Biblia husema ...
“Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa  hukiri hata kupata wokovu.” [Warumi 10: 9,10]


Ili mtu aokoke alizima... 

1. Kuamini moyoni kuwa Mungu alimfufua Yesu katika wafu.
Hii ina maana ya kuamini kazi nzima ya ukombozi wa mwanadamu ambayo Yesu Kristo aliikamilisha baada ya kufa msalabani na kufufuka siku ya tatu. Unapofika mahali pa kuyaangalia maisha yako na kuona kweli unamhitaji Yesu, basi hapo unapaswa kwanza kuamini kuwa Yesu alikufa msalabani kwa ajili yako ili upate msamaha wa dhambi.
Biblia husema.....


“Kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, Yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”

 [Matendo 16:30,31]

“Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.” [Matendo 2: 38]

Pia husema....“Huyo [yaani Yesu Kristo] manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.” [matendo 10: 43]
Amini ya kwamba Yesu Kristo alikuja duniani kwa ajili yangu na wewe ili kutupatanisha na Mungu.

 2. Kukiri kwa kinywa chako kuwa Yesu Kristo ni Bwana. 
    Baada ya kuamini moyoni mwako kwamba unamhitaji Yesu Kristo katika maisha yako, hatua inayofuata ni ya kukiri kwa kinywa chako kuwa Yesu Kristo ni Bwana. Biblia husema...“kwa kuwa kila aliitiaye jina la Bwana ataokoka” [Warumi 10:13]. Hii ni hatua ya kumuomba Yesu Kristo akusamehe dhambi zako zote na kukutakasa ili ufanyike kiumbe kipya. Ni hatua ya kumkabidhi Yesu maisha yako ili awe Bwana na Mwokozi kwako. Hii ni kwa kuwa Mwana wa Adam yaani Yesu Kristo anayo amri ya kusamehe dhambi duniani.
     Bibilia inasema hivi...“Lakini, Mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi...” [Luka 5: 24] Ndugu unaye soma somo hili kama bado hujampa Yesu maisha yako [yaani kuokoka] mtafute mtu aliyeokoka akuongoze sala ya toba au fuatisha sala hii kwa imani....

Bwana Yesu, asante kwa sababu ulikuja duniani kuwaokoa wenye dhambi ambao mmoja wao ni mimi; ulisulubiwa na kufa msalabani kwa ajili yangu ili nipate ondoleo la dhambi. Sasa niko mbele zako ee Yesu. Nisamehe dhambi zangu zote, nitakase kwa damu yako ya thamani unifanye kuwa kiumbe kipya. Futa jina langu kwenye kitabu cha hukumu, liandike kwenye kitabu cha uzima. Asante Yesu kwa kuniokoa, Amen.
 
Kama umesali sala hii kwa imani basi ujue ya kwamba Yesu Kristo sasa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Amesha kusamehe na kuzifuta dhambi zako zote. Wewe sasa ni kiumbe kipya!

3. Kuishi maisha ya kumpendeza Mungu huku ukimtegemea Yesu kama Bwana na mwokozi wako.
Mara baada ya kukiri kwa kinywa chako kuwa Yesu ni Bwana na kupokea neema ya wokovu, yakupasa kuanza safari ya “kuukulia wokovu” na kumpendeza Mungu.  Kuukulia wokovu maana yake ni kukua katika kumjua Mungu na Yesu Kristo aliye kuokoa.
Kadiri utakavyo jifunza na kukua katika kumjua Mungu pamoja na Neno lake ndivyo utakavyozidi kufanikiwa na kuiona raha ya wokovu.
Biblia husema....“Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo ya halali; mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya nini kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana.” [1Petro 4: 2 – 4]  

Maoni

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MAANA YA WOKOVU

IJUE BIBLIA - Sehemu ya I